Kante: Ukitaka ubingwa England msajili huyu jamaa
KUNA wana soka wanaamini Ngolo Kante ndio alistahili kuwa Mwanasoka Bora wa Ligi Kuu England, msimu uliopita.
Kutokana na mchango wake wa kuisaidia Leicester City kutwaa ubingwa katika msimu wa 2015/16.
Kante anacheza nafasi ya kiungo mkabaji maarufu kwa jina la `mkata umeme’ ukizungumza kwa lugha ya kimpira wa Tanzania.
Kiungo huyu ana sifa kuu mbili moja ya kukaba na kunyakua mipira na sifa nyingine ni kutibua pasi za timu pinzani.
Ingawa mashabiki wengi walimwaga sifa kwa Jamie Vardy na Riyad Mahrez kuwa ndio walichangia ubingwa wa Leicester City.
Vardy alisifiwa kutokana na umahiri wake wa kupiga mabao na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu England na pasi za hatari za Mahrez.
Mahrez ndio alipewa tuzo ya kuwa Mwanasoka Bora wa England msimu uliopita.
Hata hivyo, chati ya Kante imepanda zaidi msimu huu wakati huu akichezea Chelsea.
Si kwa sababu anaing’arisha Chelsea inayoongoza Ligi Kuu England lakini ni kutokana na jinsi Leicester City inavyoyumba.
Leicester City imegeuka kuwa kioja kutoka kwa iliyotwaa ubingwa hadi kuwa timu inayopigana kutoshuka daraja.
Kante ana umahiri mkubwa wa kuzuia mashambulizi kiasi cha kurahisisha kazi ya mabeki.
Si kwamba tu beki ya Leicester City inayoongozwa na Wes Morgan na Robert Huth inayumba pia Mahrez na Vardy wamepoteza mwelekeo wa kupachika mabao.
Chelsea sasa inafaidi fedha yake kutokana na kumnunua Kante, ambaye ameifanya kuwa moto wa kuotea mbali msimu huu.
Kiasi cha watu kujenga usemi kuwa ukitaka kuchukua ubingwa basi umsajili.
Kwani Leicester ilichukua ubingwa ikiwa na Kante lakini msimu huu sasa kibao kimegeuka kuwa Chelsea inaelekea kunyakua ubingwa ikiwa na kiungo huyo.
Kante kailetea utulivu Chelsea kwa kutibua mashambulizi ya timu pinzani na kuwafanya Diego Costa na Eden Hazard kuwa na kazi moja tu ya kuchachafya ngome za timu pinzani.
Tofauti na Leicester, ambayo kwa sasa iko taabani ikiwa pointi mbili tu juu ya timu zilizoko mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Historia ya Kante
Kante, ambaye wazazi wake wana asili ya nchi ya Mali, ana umri wa miaka 26 lakini anachezea timu ya taifa ya Ufaransa.
Alianzia soka yake katika timu ya Boulogne ya Ufaransa kabla ya kujiunga na Caen.
Mwaka 2015, alijiunga na Leicester City kwa ada ya kiasi cha pauni 5.6 kabla ya kuuzwa Chelsea kwa usajili uliogharimu kiasi cha pauni 32.
Comments
Post a Comment